VIGEZO VYA NYUMBA BORA ZA KUPANGA.

Nyumba ya kupanga ni biashara na ili iweze kuwa biashara yenye mafanikio na inayolipa inapaswa kuzingatia vigezo fulani vya kiufundi sambamba na vinginevyo vitakavyowavutia wateja tarajiwa ambao ni wapangaji kwenye nyumba husika.

Changamoto kubwa iliyokuwepo Tanzania na ambayo bado ipo kwa wengi ni mtazamo kwamba nyumba za kupanga ukishajenga tu itapata wateja kwa haraka ambao wataishi kwa muda mrefu na hivyo kazi ya mwenye nyumba ni kukusanya tu kodi na kunufaika. Katika uhalisia hili sio kweli na hasa miaka ya sasa hivi ambapo watu wameendelea nab ado wanaendelea kujenga nyumba bora za kupanga kwa kasi sana na kwa viwango bora sana kwenye mazingira yote.

Ukweli ni kwamba nyumba ya kupanga inahitaji kuwa yenye viwango fulani vya ubora ili iweze kung’ang’ania katika soko na wapangaji ambao ni makini, wasio wasumbufu na wanaoweza kuishi kwa muda mrefu kutokana na kuridhika na ubora wa kimazingira wa nyumba husika, na hata ikitokea wameondoka basi nyumba iwe inagombewa na watu wengi kutokana na viwango vya juu vya ubora ilivyonavyo, badala ya kusubiri mpaka miezi sita au mwaka mzima kuja kupata mpangaji mwingine.

Kuna vigezo vitatu muhimu vikubwa ambavyo vinaifanya nyumba ya kupanga kwua yenye hadhi na ambayo inaweza kupata wapangaji wa uhakika wasio wababaishaji na hata inapotokea wameondoka haikawii kupata wapangaji wapya.  Kigezo cha kwanza ni ubora wa kimuonekano, nyumba ya kupanga inatakiwa iwe na mwonekano unaovutia sana kwa sababu mpangaji huhusisha thamani ya muuonekano wa nyumba husika na thamani yake yeye, nyumba inapokuwa na mwonekano bora inaonekana ni ya thamani kubwa na hata mpangaji huona kwamba watu watamhesabu kama mtu mwenye hadhi ya juu kwa kuishi kwenye nyumba yenye muonekano bora. Hivyo eneo la muonekano bora wa nyumba ni muhimu sana katika kumfanya makini na mwenye uwezo kudumu kwenye nyumba husika.

Kigezo cha pili ni mpangilio bora wa kimatumizi ndani ya jengo. Hii inamaanisha kwamba mpangilio wa ndani ya nyumba kuanzai sebule, jiko, sehemu ya kulia vyumba pamoja na vyoo vinapaswa kupangilio kwa usahihi kiasi cha kuwa rafiki na kuendana na matumizi ya mpangaji. Mpangaji anapoiona nyumba huanza kuona namna ambavyo atakuwa anaitumia na hivyo kama mpangilio umekaa vibaya na hauendani kwa usahihi na matumizi ya mpangaji hilo peke yake husababisha mpangaji makini kutovutiwa na jengo hilo. Kwa mfano unakuta maliwato ipo karibu na jiko, au maliwato ipo chumbani kwenye chumba kikubwa peke yake na hivyo kulazimu watu wa nje kuingia mpaka chumbani kwenye chumba kikubwa ili kwenda maliwato, usumbufu ambao utamchosha mpangaji na kutovutiwa na nyumba hivyo.

Kigezo cha tatu ni eneo la bustani la nje. Hili ni eneo muhimu mno katika kuboresha mandhari ya eneo la nje na kuifanya nyumba kuonekana yenye hadhi kubwa sana. Moja kati ya vitu vya mwanzoni kabisa vitakavyomvutia mpangaji ni pamoja na hili la muonekano wa bora wa nje pamoja na maeneo ya bustani ambayo yanaifanya nyumba kuonekana ni ya hadhi kubwa na kutoa pia eneo mbadala la kupumzikia.

Kwa bahati nzuri ni kwamba nyumba nyingi za kupanga bado ziko katika changamoto nyingi sana kwa maana ya hadhi ya nyumba zenyewe, hivyo pale mtu utakapojenga nyumba ya kupanga yenye vigezo hivi vikubwa vitatu basi ni wazi kwamba utachukua wateja wa watu wengine ambao wameshindwa kujiongeza na kuboresha maeneo yao kwa namna itakayomridhisha mpangaji.

Karibu sana kwa ushauri zaidi.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255717452790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *