UTADANGANYWA JUU YA GHARAMA HALISI ZA UJENZI ILI UANZE KAZI.

Moja kati ya vitu vigumu sana kuwashawishi watu au wateja walio wengi ni juu ya gharama halisi za ujenzi wa nyumba wanazoazimia kuzijenga. Licha ya kwamba wengi huwa hawajui kabisa kuhusu gharama za ujenzi lakini hukataa kabisa gharama halisi za ujenzi wanazotajiwa ambazo mara nyingi huhisi na kuamini kwamba ni kubwa sana na sio za kweli bali kuna gharama nyingine ambazo ndizo za kweli.

Sasa kutokana na ukweli kwamba mtu unayetoa taarifa hiyo ya bei halisi za ujenzi huwa unapingwa na kuonekana muongo na mdanganyifu basi baadhi ya wat una baadhi ya mafundi wamejifunza na kuja na mbinu ya tofauti. Kwa kujua kwamba sio rahisi mteja akubaliane na bei halisi, kitu ambacho kitapelekea hata mtu huyo kukosa kazi hiyo basi wengi huamua kuanza kwa kutoa taarifa za uongo za makadirio ya chini sana ya gharama za ujenzi ili kumfurahisha mteja na kupewa kazi.

Kisha kazi ikishaanza na kufikia hatua kama ya pili huku wakati huo mhusika akiwa anajituma sana katika utekelezaji huku akijua bajeti aliyoisema mwanzoni haitatosha ndio sasa inambidi awe mkweli japo atatumia maneno mengi ya kupumbaza asionekane kwamba mwanzo alifanya udanganyifu kwa makusudi akiwa na malengo yake binafsi yaliyojificha. Hii mbinu huwa inasaidia baadhi ya watu hasa mafundi wa mtaalani kupata kazi angalau katika hatua za mwanzoni, ambapo hata mradi ukisimama au yeye akiondolewa katika mradi anakuwa tayari alishanufaika.

Hivyo ikiwa wewe ni mteja ambaye unataka kufahamu kila kitu katika uhalisia ili uweze kufanya maamuzi sahihi na ya uhakika basi unapaswa kufuatilia kwa umakini sana kufahamu uhalisia badala ya kutaka kusikia tu yale yanayokufurahisha. Kwa watu wengi wasio na uzoefu sio rahisi kuamini gharama za ujenzi kwa sababu huwa ni kubwa sana ukilinganisha na gharama ya vitu vingine karibu vyote vinavyohitajika na watu wa kawaida katika maisha.

Karibu sana.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255717452790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *