KWENYE UJENZI MAMBO MENGI HUYAJUI NA HAYATAKUACHA SALAMA.

Moja kati ya vitu ambavyo akili ya binadamu huwa inatugharimu navyo sana basi ni kile kitendo cha kushindwa kujua tusichojua na akili zetu kutuaminisha kwamba tunajua kila kitu kwa sababu kile tusichokijua hatukijui na wala hatufikiri kabisa kama kinaweza kuwepo. Pale tunakuwa tunajua mambo machache halafu hatujui jambo jingine lolote zaidi ya hayo machache basi akili zetu hutuhadaa kwamba hakuna cha kingine zaidi ya kile tunachojua. Hili limekuwa chanzo cha anguko la watu wengi sana.

Tunapokuja katika ujenzi watu wengi huwezi kufikiria mchakato mzima wa ujenzi tangu mwanzoni mpaka kukamilisha kama kitu ambacho kinaweza kufanyika kwa urahisi sana na kufikiri kwamba hakuna kitu cha ajabu hapo na kwamba ana ufahamu wa kila kinachokwenda kufanyika. Hii hupelekea mtu kufikiri kwamba ataweza tu kusimamia zoezi zima bila shida yoyote kwa sababu hakuna kitu chenye ugumu wala kisichoeleweka.

Na hapo ndipo wengi hufeli kwa sababu mtazamo huo husababishwa na mtu kutojua kile ambacho hajui. Ukweli ni kwamba ujenzi una mambo mengi na vipengele vingi zaidi ya ule mchakato rahisi ambao watu hufikiria. Lakini pia kuna mambo mengi sana yasiyotarajiwa hutokea katikati ya mradi ambayo huja na madhara yake yanayoathiri maendeleo ya mradi na ubora wake. Mambo haya hutokea wakati mwingine hata mtaalamu mwenyewe hawezi kuyatabiri.

Tukibaki kwenye mambo mengi, kuna vitu vingi vya kitaalamu ambavyo hutakiwa kufuata utaratibu ambapo mtu pekee ambaye anaweza kuvifanyia maamuzi sahihi ni aidha mtaalamu mwenyewe aliyefanya kazi ya michoro au mtaalamu mwingine ambaye amejifunza kazi husika kwa kina na kuielewa kwa usahihi sana ndipo huweza kufanya maamuzi sahihi yasiyokuwa na madhara hasi kwa mradi husika.

Hivyo kati ya vitu muhimu sana ambavyo havipaswi kupuuzwa au kufikiriwa kwamba havina umuhimu ni huduma za kitaalamu ambazo kazi yake kubwa ni kuhakikisha kwamba kila kitu kinafanyika kwa usahihi ili kuepuka makosa ambayo mara nyingi huja na gharama kubwa sana baadaye. Hii ni kwa sababu kuna vitu vingi sana huvijui na hujui kwamba huvijui lakini kutokujua kwako bado hakutakuacha salama bali vitakupa mshangao(surprise) ambayo hukuitarajia inayoambatana na hasara na maumivu.

Karibu sana.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255717452790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *