CHANGAMOTO MPYA KWENYE UJENZI ZITUMIKE KUUBORESHA MFUMO.

Kama tulivyoendelea kujadili kwenye makala zilizopita njia nzuri ya kupunguza makosa kwenye miradi ya ujenzi ni kuwa na mchakato maalum unaofuatwa hatua kwa hatua katika utekelezaji wa mradi wa ujenzi. Mfumo huo unatumika badala ya kutegemea maamuzi ya mtu au msimamizi mmoja ambaye ndiye anatoa maelekezo yote badala yake mchakato mzima wa utekelezaji unakuwa upo umeandaliwa tayari na kinachotakiwa ni kuufuata mpaka kukamilisha ujenzi. Mchakato huu wa utekelezaji unakuwa umeandaliwa kwa umakini sana na jopo la wataalamu ukizingatia kila hatua na umuhimu wake wa kufanyika namna hiyo iliyopendekezwa ili kufanikisha matokeo bora zaidi yanayotazakiwa.

Lakini hata hivyo pamoja na hayo tunajua kwamba katika mradi wowote ule mkubwa ambao unahusisha mfumo tata basi changamoto kujitokeza katika utekelezaji ni kitu cha kawaida na lazima kutokea. Hakuna kazi yoyote ya ujenzi iliyowahi kujengwa bila kutokea changamoto wakati wa utekelezaji wake, na hili ni bila kujalisha ni kazi ya kawaida kiasi gani. Na ndio maana siku zote utakuta mshauri wa kitaalamu anaitwa kila siku katika eneo la ujenzi kwenda kufanya maamuzi kwenye changamoto mpya iliyotokea au katika sehemu ambapo michoro haikueleza kwa usahihi nini kinachopaswa kufanyika katika hali kama hiyo.

Hivyo kwa kuwa changamoto mpya ni kitu kisichoepukika katika mradi wa ujenzi hilo halimaanishi kwamba mfumo wa utekelezaji hauna maana, kwani kupitia mfumo zile changamoto kubwa na zenye madhara makubwa zote zinakuwa zimetatuliwa au angalau zinakuwa zimetolewa maelekezo ya nini kinapaswa kufanyika ikiwa hali kama hiyo imejitokeza. Lakini habari njema ni kwamba kila changamoto inayojitokeza wakati wa utekelezaji wa kupitia mfumo kinachofanyika ni mfumo kuboreshwa hapo hapo kuhakikisha kwamba changamoto kama hiyo inapojitokeza katika hatua ya mbeleni au kwenye mradi mwingine basi inakuwa ilishatatuliwa kabla na sio changamoto tena. Kwa maana hiyo mfumo unakuwa ni bora zaidi kwa wakati huo kuliko vile ulivyokuwa kabla ya changamoto hiyo.

Kwa mfano kazi ilikuwa inaendekea katika eneo la ujenzi kisha ikatokea changamoto kwamba ramani ya msingi wa jengo kwa michoro ya uhandisi mihimili imetofautiana kidogo na ramani ya msingi kwa michoro ya usanifu wa jengo. Na kwa kuwa katika utekelezaji kwenye ujenzi watu hufuata michoro ya uhandisi mihilimili na wanapokuja kwenye mgawanyo wa vyumba ndio wanajikuta wamefanya makosa basi mfumo wa mchakato wa utekelezaji unaweza kuboreshwa kwamba. Kabla ya ujenzi kuanza kuna kipengele katika utekelezaji kwamba michoro yote ya usanifu wa jengo na michoro ya uhandisi mihimili utatakiwa kukaguliwa kama iko sahihi na inaendana kwa usahihi. Pia michoro ya usanifu yenyewe inaweza kulinganishwa kama michoro ya vipimo viwili inaendana na michoro ya picha kwa usahihi ili yasije kufanyika makosa yatakayokuja na gharama kubwa kuyarekebisha.

Kipengele hicho kitakachoingizwa kwenye mchakato wa utekelezaji wa mfumo tatizo hilo la kazi kuharibika au uzembe wa namna hiyo hautajitokeza tena ikiwa mfumo utafuatwa kikamilifu. Sasa kadiri mfumo unavyoendelea kuboreshwa kupitia miradi mingi zaidi mbalimbali ya ujenzi ndivyo kadiri unavyoendelea kuwa imara zaidi na kufanikisha kazi nyingi zaidi katika viwango bora zaidi na zaidi. Mfumo pia utasaidia ikiwa mawazo bora yanatokea katika maeneo ya ujenzi hayapotei kwani moja kwa moja yanaingizwa kwenye mchakato wa utekelezaji na hayatakaa yakosekana katika kuboresha zaidi kazi za ujenzi. Hata hivyo kwa sababu changamoto hujitokeza siku zote iwe kuna mchakato au la hakuna hasara yoyote au madhara yanayosababishwa na mchakato kwani mtaalamu wa ujenzi bado anakuwepo hivyo hakuna kinachobadilika. Lakini uzuri ni kwamba mchakato unapokuwa umeimarika hata kama msimamizi wa ujenzi hatakuwa na uwezo mkubwa sana katika kufanya maamuzi mchakato utamrahishia na matokeo bado yanaweza kuwa ni mazuri kwa sababu mfumo ndio unaofanya kazi ya kuboresha mradi wa ujenzi zaidi kuliko hata uwezo wa mtaalamu.

Karibu sana.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255 717 452 790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *