UJENZI UNATAKA UTAALAMU NA UZOEFU.

Kati ya vitu ambavyo vimekuwa vikinishangaza sana kwa muda mrefu ni jinsi kwamba kila mradi wa ujenzi unapofanyika huwa kuna makosa yanafanyika na kutakiwa kurekebishwa na kwa kutumia mtaalamu mwenye uzoefu bila kujalisha kuna fundi mjenzi mwenye uzoefu wa miaka mingapi katika utekelezaji wa mradi huo. Yaani hata unapokuta kuna umakini kiasi gani katika eneo la ujenzi kwa upande wa wale wanaojenga, hata unapokuta kuna michoro iliyokamilika kiasi gani katika eneo la ujenzi ni lazima utakuta kuna makosa ya kimaamuzi yamefanyika katika utekelezaji wa mradi husika wa ujenzi. Lakini kitu cha kushangaza ni kwamba ili kuepuka makosa hayo ilipaswa tu kushirikisha mtaalamu ambaye naye atapaswa kuweka umakini katika kazi yake ili kuepuka naye kufanya makosa.

Hii ndio sababu kwa nini nimekuwa nikisisitiza sana matumizi ya mfumo wa utekelezaji wa mradi wa ujenzi ambao unafuata mchakato wa utaratibu maalum ulioandikwa na washauri wa kitaalamu wakishirikiana na wadau wengine wazoefu katika fani ya ujenzi. Kisha mfumo huo kuanza kutumika na kuendelea kuboreshwa kadiri changamoto zinavyoendelea kujitokeza, maboresho ambayo yatakuwa yanaongezwa ili kutatua changamoto mpya zilizojitokeza mpaka inafika wakati unakuta ni nadra sana kukutana na changamoto mpya kwa sababu nyingi zilishajitokeza na kuboreshwa kwenye mfumo.

Sasa yote haya yanafanyika kutokea kwenye utaalamu na uzoefu katika taaluma husika na fani yenyewe ya ujenzi kwa ujumla. Hivyo tunaona kwamba katika mradi wowote wa ujenzi ili mambo yafanyike kwa usahihi ikiwa kuna mfumo au la, kinachotakiwa kuzingatiwa ni vitu viwili muhimu utaalamu katika taaluma husika na uzoefu katika kazi husika. Pale kimojawapo kinapokosekana katika eneo la ujenzi kati ya utaalamu na uzoefu basi husababisha makosa yenye madhara kwa mradi wa ujenzi, na pale vyote vinapokosekana basi kinachofuata huwa ni kujiandaa na hasara kubwa sambamba na majanga katika mradi husika wa ujenzi. Lakini pale vyote vinapokuwa vinapatikana basi makosa kwenye mradi husika ya ujenzi huwa ni nadra sana na yanapotokea huweza kuonekana haraka na kutatuliwa mara moja.

Hata hivyo ufuataji wa mfumo imara ambao umeboreshwa kwa kipindi kirefu huweza kusaidia kupunguza makosa kwa kiasi kikubwa sana hata kama vitu hivi viwili vimeadimika.

Karibu sana.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255 717 452 790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *