KWENYE UJENZI KUNA UJUZI/UTAALAMU NA UZOEFU.

Katika ujenzi ujuzi au utaalamu na uzoefu ni vitu viwili tofauti ambavyo vyote vina umuhimu mkubwa katika taaluma ya ujenzi kwa ujumla. Mtu mwenye ujuzi na uzoefu kwa wakati mmoja anaweza kuwa ndiye mtu sahihi zaidi na anaweza kufanya vizuri sana katika kutoa thamani ya viwango vya juu kwenye miradi ya ujenzi. Hata hivyo watu hao wenye uwezo katika maeneo hayo yote mawili huwa sio kazi rahisi sana kuwapata. Mara nyingi utakuta mtu ana ujuzi na ufahamu mkubwa sana kwenye ujenzi lakini hana uzoefu mkubwa katika utekelezaji wa shughuli za ujenzi kwa sababu hafanyi shughuli hizo moja kwa moja huku ukikuta mtu mwenye uzoefu mkubwa wa shughuli za ujenzi wa sababu anafanya shughuli hizo kila siku lakini hana ujuzi na utaalamu kamili kuweza kutegemewa kutoa maamuzi katika eneo ambalo linahitaji ujuzi sahihi wa kesi husika.

Kwenye ujenzi mara nyingi wale wataalamu kabisa kama wasanifu majengo, wahandishi mihimili wa majengo, wakadiriaji majenzi na wahandisi wa huduma kwenye majengo ni watu wenye ujuzi na taalamu husika za ujenzi ambapo huweza kufanya mambo mengi na kadiri mara zote kufanya maamuzi sahihi ya kitaaluma katika ujenzi. Lakini inapokuja kwenye uzoefu katika utekelezaji wa miradi hii utakuta wakizidiwa na wasimamizi wa ujenzi maarufu kama “site foremen” kwa sababu wasimamizi hawa ndio hufanya kazi ya utekelezaji wa kila kitu na maazimio yaliyowekwa na wataalamu wa ujenzi hivyo huweza kuweka kumbukumbu nyingi za matukio na madhara ya karibu kila kitu kinachofanyika kwenye utekelezaji wa miradi ya ujenzi. Wakati mwingine jambo hili huwachanganya sana wateja wasijue yupi hasa ndiye wa kutegemewa.

Ukweli ni kwamba wote ni wa kutegemewa na wote wana madhara pale ambapo wanakosekana kwani mara nyingi mmoja sio mbadala wa mwingine. Hata hivyo mara nyingi kama italazimu awepo mmoja ambaye ni wa kutegemewa zaidi ni mtaalamu/mjuzi kwa sababu yeye anafuata kanuni maalum ya kazi huku mzoefu akifuata vile ilivyozoeleka kufanyika huku akiwa na kumbukumbu nyingi sana za kesi tofauti tofauti za ujenzi alizokutana nazo. Hii ni kwa sababu mtaalamu ni mtu anayeweza kufanya maamuzi bila kumtegemea mtu yeyote na yakawa ni maamuzi sahihi zaidi au akaweza kufahamu mtu sahihi anayepaswa kufanya maamuzi sahihi katika eneo husika.

Hivyo ikiwa unahitaji kufahamu nani ni sahihi wa kufanya kazi hiyo jua kwamba wote ni muhimu kwa sababu mtaalamu/mjuzi atatoa miongozi na maamuzi sahihi huku mzoefu akihakikisha mambo yanatelekelezwa kwa usahihi na anapatikana wakati wote anaohitajika.

Karibu sana.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255 717 452 790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *