KWA KUJUA AU KUTOKUJUA, UNAIBIWA KWENYE MRADI WAKO WA UJENZI.

Japo ni taarifa za kusikitisha lakini pengine asilimia 90% ya mafundi wa kujenga hufanya wizi na udanganyifu kwenye miradi ya ujenzi kwa manufaa binafsi ya moja kwa moja au yasiyo ya moja kwa moja. Hata hivyo kutokana na mahusiano na imani ambayo hujengeka kati ya mteja na fundi wake wa kujenga huwa ni vigumu sana mtu kujua kama kuna namna yoyote fundi huyo anakuwa amemwibia au la. Lakini ukweli ni kwamba japo sio rahisi kuamini lakini mara nyingi utakuta kuna namna fundi huyo amefanya udanganyifu. Hii ni kwa sababu huo hasa ndio utamaduni halisi wa mafundi walio wengi ambao umefanywa kama vile ni jambo sahihi la kufanya.

Changamoto kubwa iliyopo ni kwamba sio rahisi mtu kuelewa pale unaibiwa kwa sababu kwanza unamuamini sana yule ambaye huenda anakuibia au anafanya udanganyifu, pili utakuta kuna maeneo mengi sana anakueleza ukweli kwa mifano hai kabisa na kitaalamu sana kiasi kwamba kwa lile eneo ambalo anafanya udanganyifu sio rahisi kulifahamu. Jambo la tatu ni kwamba hata ikitokea umeanza kupata mashaka huwa anakuwa na sababu za msingi sana za kitaalamu kwa nini kile anachokushauri ni muhimu na kinastahili kufanyika kwa namna hiyo aliyochagua yeye.

Jambo la nne ni kwamba mambo mengi unayoambiwa ni mapya kwako hufahamu chochote mpaka ufanye ufuatiliaji ili uweze kugundua kitu ambacho mara nyingi hutafanya na hata ikitokea umefanya tayari ameandaa majibu ya kukupa ambayo yatakuwa yanaingia akili kwako. Pia mambo ya kufuatilia ni mengi sana na wewe labda kama una kumbukumbu kali sana kwani hata siku nyingine ukija kukutana na vitu hivyo hivyo unaweza usikumbuke hata alikwambia nini wakati mlipokuwa mnafanya kazi hiyo. Kwa kifupi watu wana akili na ujanja mwingi sana linapokuja suala la kufanya udanganyifu katika mambo ya kiufundi ili kutimiza malengo yao kwako.

Dawa pekee ya kuepuka kukutana na udanganyifu na kuibiwa ni kuhakikisha unatafuta watu ambao wana sifa ya uaminifu usiotilia mashaka na kufanya nao kazi. Unapofanya kazi na watu ambao sio waaminifu na wanalenga kukuibia sio rahisi ufanikiwe kuwakwepa hasa kama hufahamu tabia zao ambazo hata hivyo sio rahisi kuzifahamu kiurahisi. Unaweza kufikiri una akili sana za kuwakwepa na kuhisi umefanikiwa kumbe wao walishakupatia na kukuibiwa na wala huna habari kabisa kwani mbinu za kuibiwa ni nyingi sana.

Karibu sana.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255 717 452 790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *