KWA NINI WIZI WA VIFAA VYA UJENZI NI MKUBWA SANA KATIKA MAENEO YA UJENZI?

Kama wewe sio mtu wa kujishughulisha na shughuli za ujenzi au hujawahi kujihusisha na uuzaji wa vifaa vya ujenzi unaweza usijue ni kwa kiasi gani wizi wa vifaa vya ujenzi ni mkubwa sana kwenye miradi ya ujenzi. Kimsingi wizi wa vifaa vya ujenzi ni mkubwa sana kwenye miradi ya ujenzi kuanzia ule wizi wa moja kwa moja na usio wa moja kwa moja. Lakini baadhi ya watu wanajiuliza ni nini kinapelekea wizi huu kuwa mkubwa kiasi hicho na wa uhakika kiasi hicho? Nini kinachowasukuma watu kujihusisha na vitendo hivi vinavyohatarisha kazi zao n ahata kuharibu majina yao lakini bado wako tayari kufanya hivyo tu?

Sababu ya kwanza ni lazima tukubali kwamba ni mtazamo na  utamaduni uliojengeka wa kukosekana kwa uaminifu uliopo kwenye jamii zetu na hususan jamii ya kitanzania ambapo mtu unapopata nafasi ya kunufaika kifedha na mali kwa kupitia wizi au ufisadi na usifanye hivyo unaonekana mjinga au mshamba. Yaani mtu anapopata mafanikio kwa kupitia wizi na ufisadi anaonekana ni shujaa na watu wanamsifia na kuchukulia kama mfano wa mtu “mjanja” aliyeweza kupata mafanikio kwa njia hizi. Hizi ni taarifa za kusikitisha sana lakini ndio sababu mama na chimbuko la sababu nyingine zote zinazoambatana na sababu hii. Mtazamo huu potofu unasababishwa pia na watu kuamini kwamba kuna uhaba wa fedha na fursa na kufanikiwa bia kuiba ni kitu kisichowezekana hivyo inapotokea fursa ya kuiba ili kutajirika sio ya kuiachia.

Sababu ya pili ni faida kubwa ambayo ipo katika wizi wa vifaa vya ujenzi. Wote tunajua kwamba vifaa vya ujenzi kwa ujumla ni vya gharama kubwa sana na wakati watu wengi sio watu wenye vipato vikubwa sana hasa wafanyakazi au mafundi katika sekta ya ujenzi hivyo anapofanya tukio moja la wizi linaweza kumpa faida ya kifedha ambayo angeweza kutumia hata miezi miwili akifanya ufundi kuipata. Yaani manufaa ni makubwa sana kiasi kwamba mtu anapopata fursa ya kufanya wizi anashawishika kiurahisi kuchukua fursa hiyo. Kwa mfano mtu akifanikiwa kutorosha nondo 20 pekee anaweza kutengeneza mpaka zaidi ya Tshs 500,000 kwa mara moja. Hapo bado akitorosha tena mifuko kadhaa ya saruji ni Tshs 500,000 nyingine, akifanikiwa kuchakachua kokoto na kutorosha mita kadhaa za ujazo ni Tshs 500,000 nyingine kwa wakati mmoja. Hivyo unakuta manufaa anayopata ni makubwa sana kuliko vile anavyoweza kufanikiwa kupitia ufundi, wakati huo huo akiwa na imani kwamba hawezi kujulikana.

Sababu nyingine inayochochea wizi wa vifaa vya ujenzi ni urahisi uliopo katika kuuza vifaa hivyo. Mara nyingi vifaa vinavyoibiwa huenda kuuzwa kwenye maduka ya vifaa vya ujenzi au kwenye stoo kwa bei ambayo inaleta faida kubwa kwa mfanyabiashara. Wote tunajua kwamba kila mtu anataka kupata faida kwenye biashara yake hivyo mfanyabiashara anapopata bidhaa za gharama nafuu sio rahisi kuziachilia kwa sababu kwanza mara nyingi wala haambiwi kwamba vimeibiwa bali vimebaki tu kutoka kwenye mradi wa ujenzi uliokuwa unaendelea. Hivyo vifaa vinapoibiwa tu huwa vinapata soko haraka na kwa urahisi sana ndio maana watu hushawishika kuiba kwa haraka kwa sababu wanajua hawatapata shida kwenye kuuza na kupata fedha kwa haraka.

Hivyo ni muhimu sana mtu kuchagua watu waaminifu wa kufanya nao kazi kwani kudili na watu wasiokuwa waaminifu ni kazi ngumu na watakuyumbisha sana.

Karibu sana.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255 717 452 790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *