WIZI WA VIFAA VYA UJENZI KWENYE MRADI WA UJENZI.

Katika nchi ambayo bado maeneo mengi hakuna mifumo imara sana ya udhibiti na katika jamii ambayo imeharibika kimaadili hasa katika yale maadili ya msingi kama hizi nchi maskini za kiafrika basi moja kwa moja unategemea kwamba tabia kama wizi kwenye eneo la ujenzi itakuwa ni kubwa. Ukweli ni kwamba wizi kwenye ujenzi ni kama utamaduni wa mafundi, tabia hii imezagaa sana japo haizungumzwi kwa ukubwa na uzito inayoleta lakini madhara yake ni makubwa sana, yanaumiza sana watu na yanarudisha sana nyuma maendeleo ya watu.

Changamoto kubwa sana ya tabia hii ya wizi kwenye eneo la ujenzi hasa katika miradi midogo na ya watu binafsi ambayo pia ndio inaendeshwa bila mfumo madhubuti wa udhibiti wala uwajibikaji unaosimamiwa na sheria ni kwa unaanzia kwenye mtazamo. Mtazamo uliojengeka kwa watu wasiojali na wasio na malengo yoyote makubwa kwenye maisha ni kwamba katika maisha yake hataweza kufanikiwa bila kuwa mwizi. Msamiati wa uadilifu kwenye akili zao haupo kabisa kwa sababu tayari umeondolewa na mtazamo huu wa kwamba hatua kubwa kwenye maisha yake au ndoto zake atazifikia kupitia wizi, hivyo wizi ni changamoto sugu katika eneo hili.

Wote tunajua kwamba hakuna kitu kigumu kumbadilisha binadamu kama mtazamo ambao ndio unaathiri tabia ya mtu na unapelekea matendo yake katika yale anayofanya. Mtu wa namna hiyo anapewa dhamana kubwa ya kusimamia mradi kama ujenzi ambao unahusisha pesa nyingi sana katika utekelezaji wake kuanzia vifaa mpaka ufundi. Mwisho wake sasa hapo ndipo unakutana na majanga makubwa. Sasa linapokuja suala la wizi kwenye mradi wa ujenzi kutokana na mtazamo wa watu hasa mafundi jinsi ulivyo kinachofuata baada ya hapo ni ubadhirifu mkubwa kwenye mradi ambao unapelekea aidha hasara kubwa kwa mteja au udhaifu wa jengo lenyewe au vyote viwili kwa pamoja.

Hapa sasa unajiuliza nini kifanyike ili kukabiliana na wizi ikiwa huo ndio mtazamo wa mafundi karibu wote kwenye eneo la ujenzi. Baadhi ya watu huwa wanajidanganya kwamba akiweka mtu wake wa karibu au mtu anayependekezwa kwake kwamba anaweza kumsaidia kusimamia ujenzi huo basi atakuwa ametatua tatizo. Anachokuja kugundua akiwa ameshachelewa ni kwamba yule mtu wa karibu ambaye wakati mwingine ni ndugu yake wa damu ndiye mwizi kushinda hata hao mafundi aliowaweka. Hii ni kwa sababu kwanza mtu huyo unakuta alikuwa hana kazi ya kufanya hivyo hana njia yoyote ya kumwingizia kipato au angalau hana njia ya kumwingizia kipato cha maana kinachojitosheleza, na kawaida ya binadamu tumeumbiwa sana tamaa hasa watu wasiojua kujihangaisha ambao huamini katika njia ya mkato. Kwa sababu tamaa ina nguvu kubwa sana ndani ya mtu basi huyo aliyeaminiwa anaishia kuwa mwizi mkubwa kuliko hata wale mafundi kwa sababu hana hata kipimo cha kudhibiti kile anachoiba ukilinganisha na madhara yake kwenye ujenzi husika. Watu wengi wameumizwa sana kwa njia hii.

A ‘Danger, Construction site, Unauthorised Persons Keep Out’ sign mounted on a wire fence in front of a building site

Lakini pamoja na yote hayo bado hakuna changamoto inayokosa suluhisho, inaweza kuwa sio njia iliyozoeleka na wengi lakini ili kuepusha upotevu wa muda na hasara kubwa kwenye ujenzi ni vyema ukafanya kazi na kampuni ndogo inayokua ambayo bado haitozi gharama kubwa kutoa huduma ya ujenzi. Gharama za kampuni ndogo huwa zinakaribia kulingana na gharama za mafundi wa mtaani lakini wakiwa wanasimamia ubora na uaminifu wa mradi kwani wanajua kwamba wana malengo makubwa watawajibika kwa chochote kitakachoharibika kwenye mradi. Hata hivyo kushirika kampuni ndogo pekee haitoshi bali unapaswa pia kusaini mkataba wa kazi ambao utaweka masharti ya kufanya ukaguzi wa maendeleo ya mradi na mwisho wa mradi kuona kama yale mliyokubaliana yametimizwa na makadirio ya vifaa yaliyotumika yanaendana na fedha iliyotolewa.

Kufanya kazi na kampuni ndogo inayokuwa na inayojenga misingi sahihi ya ujenzi kwa kuzingatia pia mikataba sahihi kutakuondolea usumbufu mkubwa, hasara na majuto mengi ambayo ungepaswa kukabiliana nayo kama ungefanya mradi huo kienyeji. Lakini pia kampuni ndogo inasimamia utaalamu na kuhakikisha kwamba jengo linajengwa kwa kuzingatia viwango bora na vinavyokubalika sambamba na kukupa ushauri sahihi kwenye kila hatua. Kampuni ndogo pia itakusaidia kukupa ushauri sahihi katika kila hatua sambamba na kukushauri namna ya kuepuka adhabu zinazotolewa na mamlaka mbalimbali za ujenzi kwa mtu kukwepa au kupuuza miongozi mbalimbali inayotolewa na mamlaka hizo.

Karibu sana.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255 717 452 790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *