KWENYE UJENZI WIZI NI UTAMADUNI KWA MAFUNDI.

Kwa watu ambao ambao wameshafanya ujenzi mara kwa mara wengi jambo hili limekuwa likiwashangaza kidogo, yaani sifa kuu waliyonayo mafundi wengi kwenye ujenzi ni kufanya wizi au udanganyifu kwa kila nafasi wanayopata. Hili limekuwa likiwashangaza wengi lakini ndio uhalisia, yaani kila nafasi inayopatikana ya kufanya wizi na udanganyifu basi huwa inatumiwa vizuri bila mtu kujali chochote. Kuna siku nilikuwa nimeenda kwenye eneo la mteja wetu mmoja kupima kabla ya kuanza kazi ya kuchora ramani husika tukawa tunajadili juu ya ujenzi wa mradi wake huo. Hivyo tukawazungumzia mafundi nikamwambia ni muhimu kuwa makini kwa sababu mafundi wengi sio waaminifu hivyo anapaswa kutafuta mtu mwaminifu kuhakikisha kazi yake inafanyika kwa viwango bora, alinijibu akaniambia “hakuna fundi mwaminifu”.

Hata hivyo japo binafsi naamini wapo wachache sana waaminifu lakini maoni ya baadhi ya watu ambao walishaibiwa yanaweza kukuonyesha ni jinsi gani hali ni mbaya sana. Ukweli ni kwamba tabia ya wizi kwa mafundi imeshakuwa ni utamaduni wao kwa sasa kutokana na jinsi mitazamo yao kwa ujumla inavyoamini katika wizi ni vile wanavyoamini kitu pekee kitakachowatoa kwenye maisha ni wizi. Utamaduni huu umekuwa na nguvu sana kwa mafundi kiasi kwamba anapotokea fundi ambaye haibi anaonekana aidha ni mjinga au ni mzembe sana kwa kuchezea nafasi ambayo huenda ndio ya kumtoa kimaisha, hivyo hata wale ambao hawana nia wala mtazamo huo wanajikuta wameshajiingiza kwenye tabia hizo ambazo huendelea kuwa utamaduni wao siku hadi siku. Kwa unakuta sasa utamaduni wa mafundi wote kwa ujumla ni kwamba inapotokea nafasi ya kufanya wizi na udanganyifu hupaswi kabisa kuiachia.

Utamaduni huu wa wizi ambao baadhi hufanyia kama utani kwamba uko ndani yad amu kabisa ya mafundi umesababisha hasara, maumivu na hata magonjwa ya moyo kwa watu mbalimbali walioumizwa na mtazamo huu mbaya. Hata hivyo kuna wengine ni kama hujitakia tu kwa sababu wakiambiwa kwamba mafundi ni wezi huamini kwamba yule wa kwake hawezi kumwibia au mbaya zaidi huleta ndugu yake amsaidia kumsimamia ujenzi akiamini kwamba kwa sababu ni ndugu yake au ni mtu wa karibu basi hataiba. Lakini changamoto huja pale ambapo ndugu huyo anakuja kushawishiwa na watu wengine namna anaweza kunufaika kwa kumwibia ndugu yake na jinsi anavyochezea nafasi hadimu ya kutokufanya hivyo.

Suluhisho pekee la kudhibiti wizi na ubora katika miradi ya ujenzi ni kutumia mifumo na mikataba itakayopelekea uwajibikaji kisheria kwa pande zote mbili ambayo humweka mtu katika nafasi ya kuhakikisha yeye mwenyewe anaweka bidii katika kulinda kile ambacho huenda angekiiba kama mazingira yanamruhusu. Lakini muhimu zaidi ni kuhakikisha mtu unatumia kampuni ndogo isiyo na gharama kubwa wala masharti makali sana ambayo mtu huwezi kuyamudu kwa ngazi yako ya mradi na kipato. Bila kufanya hivyo utaibiwa ambapo ikiwa utaibiwa sana unaweza kugundua lakini ikiwa wanaokuibia watakuwa makini vizuri kucheza na akili zako sio rahisi ugundue na ujenzi ukiisha basi unasahau moja kwa moja.

Karibu sana.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255 717 452 790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *