KUJENGA MRADI MDOGO, KWA NINI KAMPUNI NDOGO?

Katika makala zilizopita nimeeleza sana kuhusu changamoto za ujenzi ambapo changamoto mbili kuu zimekuwa ni uaminifu na ubora. Watu wengi ambao bado hawajawahi kufanya ujenzi kwenye maisha yao wanaweza wasielewe kwa uzito unaostahili kuhusu changamoto hizi sugu sana ambazo zinaumiza sana watu kila siku. Watu ambao wameshapitia maumizi ya kuibiwa au kuharibiwa kazi au vyote viwili ndio wanafahamu kwa usahihi ni kiasi gani hizi ni changamoto kubwa sana. Watu wengi na hasa katika nchi hizi zenye maskini wengi, wajinga wengi na watu wasiokuwa na misingi yoyote ya kimaadili wanayoisimamia viwango vya udanganyifu na wizi viko juu sana. Yaani ni vigumu sana kupata mtu anayeweza kusimamia jambo lenye maslahi ndani yake kwa uaminifu unaotakiwa bila kufanya uharibifu na wizi wa rasilimali kwa namna tofauti tofauti.

Kuna watu wengine wanadhani kwamba wao ni wajanja sana hawawezi kuibiwa au wao walifanikiwa kujenga bila kuibiwa kwa hiyo suala la wizi na udanganyifu haliwahusu. Kitu ambacho watu hawa hawajui ni kwamba kwanza kuhusu kuibiwa mpaka makampuni makubwa yanaibiwa na wafanyakazi pale yanapokosa umakini, yaani ni suala la upenyo kidogo tu mtu ameiba. Makampuni haya yana uzoefu mkubwa na mafundi kwa miaka mingi sana lakini bado yakijisahau yanaibiwa hivyo suala la kuibiwa sio jambo rahisi sana kulidhibiti hasa unapokuwa ni mgeni kwenye sekta ya ujenzi. Lakini pia kuna kuibiwa bila kujua kama umeibiwa, na hili ndio jambo ambalo hutokea watu wengi kwani sehemu kubwa ya wizi uliofanyiwa unaweza usije kugundua kabisa kwani ni jambo lililopo nje ya uwezo wako kufahamu.

Sasa udanganyifu na wizi ndio hupelekea kukosekana kwa ubora na viwango sahihi katika ujenzi, lakini kwa bahati mbaya hata viwango vyenyewe kutokuwa katika ubora sahihi bado mtu anaweza asifahamu kwa sababu ya kukosa uzoefu. Hivyo kudili na watu kwenye sekta ya ujenzi ni changamoto kubwa na ambayo inahitaji mbinu na mikakati mikali kukabiliana nayo kitu ambacho mtu binafsi peke yake bado anaweza asiweze. Nasema mtu binafsi itakuwa ngumu kufanikisha hilo katika mazingira ya kawaida kwa sababu kwa uzoefu tu watu wengi ambao hukutana na mtu asiye mwaminifu huamini kwamba ni huyo pekee ndiye sio mwaminifu lakini kuna wengine ambao ni waaminifu au akimtumia ndugu yake au mtu mwingine wa karibu basi atakuwa ametatua changamoto ya kukosekana kwa uaminifu. Kinachotokea ni anakuja kugundua kila anayemchukia tabia ni zile zile na hata mpaka ndugu, jamaa na marafiki tabia ni hizo hizo lakini akiwa ameshachelewa. Ni vigmu sana kupata mtu ambaye ni mwaminifu lakini unachoweza kupata ni mtu ambaye ana akili sana kiasi cha kuiba bila kujukulikana.

Hapa sasa ndipo umuhimu wa kufanya kazi na kampuni ndogo unaingia. Siwezi kusema kwamba kampuni ndogo ndio waaminifu sana, hapana kwani kampuni nazo zinaendeshwa na watu ambao nao ni binadamu wenye malezi na tabia mbalimbali zisizofaa. Lakini kampuni ndogo ikishaamua kuwa ni kampuni inakuwa na kanuni zake za uendeshaji inazozisimamia ambazo zinailinda kampuni dhidi ya kuchafua jina lake. Lakini pia ukifanya kazi na kampuni ndogo ambayo inaendeshwa na watu wenye akili zaidi unaweza kuwataka kukupatia mkataba ambao utalinda maslahi yake kwenye mradi sambamba na kukuepesha na uharibifu unaoweza kuletwa na wizi na uzembe. Mkataba huu utasaidia kukupa nguvu ya kisheria ya kuiwajibisha kampuni pale utakapogundua umefanyiwa ubadhirifu wa namna yoyote ile.

Kwa upande wa gharama pia kampuni ndogo huwa hazina gharama kubwa sana ukilinganisha na kutumia mafundi au mtu mmoja mmoja hivyo unakuwa huingia gharama kubwa sana lakini unapata huduma bora na za uhakika. Kampuni ndogo zikiwa zinajenga jina kabla hazijawa kubwa na kuwa na gharama kubwa sana ni sahihi zaidi kutumia kwani pia zinakuepushia usumbufu mkubwa kwenye kufanya ufuatiliaji wa mambo ambayo itabidi uhangaike nayo sana wakati ujenzi unaendelea ambayo yatakugharimu muda wako mkubwa na hata gharama ambazo zitatokana na kukosa uzoefu kwa jambo husika. Kampuni ndogo itakurahisishia kufuatilia taratibu zote zinazohitajika na mamlaka za ujenzi katika kutimiza vigezo vya kuendelea kwa sababu ya uzoefu walionao kwenye sekta ya ujenzi.

Karibu sana.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255 717 452 790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *