FUNDI UJENZI HAWEZI KUZIBA NAFASI YA MSHAURI WA KITAALAMU KWENYE UJENZI.

Licha ya kwamba siku hizi miradi mingi ya ujenzi inahitaji mpaka ukamilishe michoro ya ramani kwanza kisha ndio ukaombe kibali kwenye halmashauri ya mji, manispaa au jiji kwanza ndio uruhusiwe kuanza ujenzi hasa kwa maeneo yote ya mjini lakini bado kuna watu wengi wanaamini baada ya kupata kibali cha ujenzi inabidi utafute fundi wa kawaida wa mtaani umpe kazi yote afanye mwenyewe. Huu umekuwa ni mtazamo na imani ya wengi kwa sababu kwanza ndio mazoea yaliyopo kwenye ufundi wa ujenzi tangu miaka mingi lakini zaidi ni imani na mtazamo kwamba mafundi wana gharama ndogo na wahandisi wa kampuni wana gharama kubwa hivyo kutumia mafundi.

Kwanza kabisa inapaswa ifahamike kwamba fundi yeyote bila kujali amefanya kazi kwa miaka mingi kiasi gani bad ohana uwezo wa kusimamia kazi ya ujenzi kwa usahihi bila kufanya makosa mengi ya kitaalamu kutokana na yeye kutokuwa na uelewa sahihi wa kitaaluma kwa kazi husika. Binafsi kwa miradi yote ya ujenzi niliyotembelea isiyokuwa na usimamizi sahihi wa kitaalamu nimekuta kuna makosa mengi yamefanyika kwa sababu ya kukosekana mtu mwenye elimu maarifa sahihi ya usanifu majengo au uhandisi kwenye kufanya maamuzi kwenye hatua husika ya mradi huo. Hilo hupelekea miradi kuwa na changamoto mbalimbali au kutojengwa katika viwango sahihi lakini mtu wa kawaida asiye na maarifa husika hawezi kuona wala kuelewa kwa usahihi isipokuwa tu kuna vitu vitakuwa haviko sawa ambavyo vinapunguza hadhi na thamani ya jengo hilo na hata kuathiri matumizi yake.

Kwa majengo makubwa changamoto hii hutatuliwa kiurahisi kwa mradi kulazimika kusajiliwa kwenye bodi za ujenzi ambazo huweka taratibu za kufuatwa ambazo huhakikisha mradi umefanyika kwa kuzingatia wataalamu wa aina zote na hivyo kwa sehemu kubwa mradi huo hujikuta ukipunguza sana makosa. Lakini kwa miradi midogo au ya watu binafsi isiyo na msukumo mkubwa kutoka kwenye mamlaka hutegemea maamuzi binafsi au busara ya mmiliki au mteja wa mradi husika kujiamulia amtumie nani kwenye utekelezaji wa ujenzi. Hivyo hapo itategemea na uelewa na umakini wa mteja kwenye kuamua maamuzi sahihi ya kufanya katika kesi hiyo.

Changamoto kubwa mbili za mafundi kwenye miradi ya ujenzi ukiondoa wizi na udokozi wa vifaa vya ujenzi huwa ni moja kukosa uelewa sahihi wa kitaaluma kwenye kile anachofanya zaidi ya kuzoea utekelezaji pekee hivyo kupuuza baadhi ya vitu muhimu na mbili ni kukosa busara ya kimaamuzi kwa kushindwa kuangalia mbali kwenye safari ya jengo hilo badala yake kuangalia maslahi ya haraka au urahisi wa yeye kumaliza kazi. Mambo haya huonekana dhahiri sana mara zote ambazo huwa ninatembelea site za ujenzi kukagua ili kupitisha au kusimamisha kazi ikiwa kuna vitu vinafanyika isivyotakiwa. Kwa kushindwa kufanya maamuzi sahihi hadhi na thamani ya mradi hushuka sana kwa sababu ndio uwezo, akili na busara ya kimaamuzi huwa imeishia kwa fundi husika. Kwa hiyo inapaswa kuhusisha wataalamu wote kwenye jengo kwani gharama ya kuwalipa ndogo ukilinganisha na thamani wanayoitoa ambayo inaweza isionekane kiurahisi lakini pia gharama hizo bado ndogo sana ukilinganisha na gharama za ujenzi wenyewe.

Kwa upande wa gharama kwa miradi midogo gharama za mafundi na gharama za kampuni ndogo kwa mradi husika huwa hazitofautiana sana tena wakati mwingine unaweza kukuta fundi ana gharama kubwa zaidi kwa jinsi anavyojiwekea bei yeye mwenyewe. Suala kwamba mafundi wana gharama ukilinganisha na kampuni ni imani tu iliyojijenga kwa watu kwa sababu wakisikia mtu ni mhandisi wanamuogopa na kumhofia lakini hana gharama kubwa kwa mradi wa kawaida. Saa nyingine kampuni huwa na gharama ndogo zaidi kwa sababu inakuwa na miradi mingi hivyo inakuwa rahisi kwao kupata faida kutokana na kupunguza gharama kwa sababu ya ukubwa wa uendeshaji wa kazi hizo. Hilo limetokea mara nyingi ambapo kampuni yetu imekuwa ikipeleka maombi ya kufanya mradi fulani na kukuta mafundi wa kawaida wakiwa wameweka gharama kubwa kuliko kampuni. Hivyo unakuta bado manufaa ya kufanya kazi bila wataalamu na mafundi pekee ni gharama kubwa kuliko hata ukifanya kazi na kampuni kama ya kwetu lakini ukiwa na uhakika wa kupata huduma bora iliyoongezwa thamani ambayo imejumuisha wataalamu wote na mchakato muhimu kuzingatiwa.

Karibu tuwasiliane na kufanya kazi pamoja kwa mawasiliano hapa chini.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255 717 452 790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *